CONTACT SUPPORT
+255746984100 / +255784108800
Tanzania

SHIRIKA LA NDEGE LA PRECISION AIR KUZINDUA KITUO CHA MAFUNZO

 Januari 20, 2021 Dar es Salaam, Tanzania. Shirika la ndege la Precision Air limetangaza kufungua kituo chake cha mafunzo ikiwa ni baada ya kupata kibali cha kuendesha kituo cha mafunzo kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Kituo hicho cha mafunzo kinatarajia kutoa mafunzo kama; Kozi ya awali ya wahudumu wa ndege, Kozi za usimamizi wa rasilimali watu katika uhudumu wa ndege, kozi ya usafirishaji wa mizigo hatarishi kwenye ndege, Kozi ya usalama wa anga na Kozi ya uzito na usawa wa ndege.

Mkurugenzi Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Precision Air, Bwana Patrick Mwanri akizungumza na vyombo vya habari amesema kuwa kuanzia tarehe 1 Machi 2021 kituo hicho kitaanza rasmi kwa kuanza na mafunzo ya wahudumu wa ndege.

 “Tunafurahia mafanikio haya na tumeazamia kuzalisha wafanyakazi mahiri wa tasnia ya anga nchini na nje ya mipaka ya Tanzania. Tunauzoefu wa kutosha katika tasnia ya anga na ni lengo letu kuutumia uzoefu huo katika kufundisha Watanzania ambao wataziba pengo la taaluma katika tasnia ya anga nchini Tanzania.Tumezalisha wafanyakazi wengi kwenye sekta, waliowahi kupitia Precision Air ambao hivi sasa wako katika mashirika na kampuni mbali mbali ya kitaifa na kimataifa, hii inatupa kujiamini kuwa tunaweza kutoa watalaamu mahiri wa sekta ya anga.” Aliongeza.

Kituo hicho ambacho kitakua katika makao makuu ya shirika hilo yaliyoko Jijini Dar es Salaam sasa kinapokea maombi kwa wanafunzi wenye kukidhi vigezo. Hali kadhalika katika taarifa hiyo kwa vyombo vya habari uongozi ulidokeza kuwa mafunzo mengine tofauti na uhudumu wa ndege yatatolewa kulingana na maombi kadri yatakavyokuwa yakipokelewa.

“Kituo chetu cha mafunzo siyo tu kwa ajili ya wanafunzi wanaoaanza lakini pia tunatoa mafunzo kwa wafanyakazi walio kazini katika sekta ya anga. Tumejipanga kutoa mafunzo yenye hadhi ya kimataifa na tunapokea maombi ya mafunzo kutoka mashirika mengine pia”Bwana Mwanri alieza zaidi.

Kituo cha Mafunzo cha Precision Air kimeanzishwa na kitaendeshwa na Shirika la ndege la Precision Air na kimepat usajili namba CAA/ATO/003 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania.

Precision Air ni shirika la Kitanzania linalotoa huduma za usafiri wa anga kutoka katika makao yake makuu Dar es Salaam, kwenda sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi ikiwemo; Arusha, Bukoba, Dodoma, Kahama, Kilimanjaro, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Zanzibar na Nairobi. Shirika hilo pia linatoa huduma zingine ikiwa ni pamoja na huduma kukodisha ndege, matengenezo na usafirishaji wa mizigo kwa njia ya anga.

We are using cookies to personalize and enhance your use of the Precision Air Website. By continuing to use our website without changing your cookie settings, you are agreeing to the use of cookies as set in the Precision Air Privacy Policy.