TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI PRECISION AIR YAREJESHA SAFARI ZAKE ZA KAHAMA NA TABORA

Dar es Salaam, Alhamisi, Mei 16 2019 Baada ya abiria kusubiri kwa hamu, hatimye shirika la ndege la Tanzania la Precision Air limerejesha safari zake za kuelekea wilayani Kahama na,mkoani Shinyanga na Tabora.

Precision Air itakua ikifanya safari zake mara tatu kwa wiki, siku za Jumapili, Jumatano na Ijumaa kuelekea wilayani Kahama na Tabora kutokea Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu kurudi tena kwa safari hizo, Meneja wa Masoko na Mawasiliano, Bw.Hillary Mremi amesema, “Precision Air inatambua umuhimu na mchango wa wilaya ya Kahama na mkoa wa Tabora kwenye shughuli za kibiashara,Kilimo na uchimbaji madini mkoani, hivyo tunategemea kwamba kurejea kwa safari hizi kutasaidia katika kuendeleza shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara,kilimo na uchimbaji madini mkoani humo.”

Aliendelea kusema, “Sasa kutakuwa na urahisi wa watu na mizigo kusafiri kwenda maeneo mbali mbali ndani na nje ya mikoa hiyo, hali kadhalika muunganiko rahisi kwenda kwenye bandari kavu iliyoko Isaka ambayo, pia huunganisha na kutumiwa na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Congo (DRC). Napenda kuchukua nafasi hii kuwasihi wafanyabiashara wote wakubwa kwa wadogo kutumia fursa hii ipasavyo.”

Kuhusu Shirika la Ndege la Precision Air

Precision Air ni shirika la umma lililoanzishwa mnamo mwaka 1993 na linatoa huduma za usafiri wa anga kwenda sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi. Safari zake huanzia makao yake yaliyoko makuu Dar es Salaam kuelekea Arusha, Kilimanjaro, Serengeti, Mtwara, Kahama, Bukoba, Mwanza, Zanzibar, Tabora, Serengeti, Nairobi, Entebbe na makao makuu ya nchi Dodoma. Huduma nyingine zinazotolewa na shirika ni pamoja na huduma za ubebaji mizigo kwa njia ya anga. Hali kadhalika shirika la Precision Air limewahi kupokea tuzo kadha wa kadha kutoka Tanzania Society of Travel Agents, Africa Aviation News Port, Tanzania Leadership Awards, TASOTA, na pia kampuni ni mshirika wa Soko la Hisa la Dar es Salaam.